Tuesday, June 21, 2011

SPIKA ANAPENDELEA MAWAZIRI, SERIKALI: ANAKIUKA KANUNI ZA BUNGE!

TAARIFA KWA UMMA

Dodoma, Juni 17, 2011

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeelezea kusikitishwa na namna ambavyo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano amekuwa akishughulikia mijadala ya masuala muhimu kwa umma na ambayo yanaelekea kuibua uozo katika utendaji wa Serikali na watendaji wake wakuu.

Hii inafuatia uamuzi wa Spika kukataa maswali aliyoulizwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu mauaji ya wananchi wengi wa vijiji vinavyozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime yaliyofanywa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Polisi ya Tarime na Rorya kwa vipindi tofauti tangu mwaka 2008.

Maswali hayo yaliulizwa na Mheshimiwa Tundu Lissu (Singida Mashariki, CHADEMA) na Mheshimiwa Esther Matiko (Viti Maalum, CHADEMA) wakati wa Kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu katika Kikao cha Tisa cha Bunge la Jamhuri siku ya Alhamisi ya tarehe 16 Juni 2011.
Hata hivyo, katika hatua ya kushangaza, Spika wa Bunge alikataza maswali hayo kujibiwa kwa hoja kwamba yalikuwa yanahusu mambo ambayo tayari yako mahakamani na kwa hiyo kuyajadili Bungeni itakuwa sawa na kuingilia uhuru na mamlaka ya Mahakama kinyume na kanuni 64(1)(c) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007.

Alipoombwa mwongozo wake kutokana na ukweli kwamba hakuna kesi hata moja ambayo imefunguliwa au inayoendelea katika mahakama yoyote ya Tanzania inayohusu mauaji ya wananchi wa Nyamongo au yanayowahusu polisi wanaohusika na mauaji hayo, Spika Anna Makinda alidai kwamba wauliza maswali wenyewe walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime yanayotokana na matukio ya mauaji ya wananchi watano yaliyofanywa na polisi katika eneo la Mgodi wa North Mara tarehe 16 Mei mwaka huu na kwa hiyo hawakupaswa kuuliza maswali yao.


Akizungumzia uamuzi huo wa Spika Makinda, Mbunge Lissu - ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni - alimtuhumu Spika Makinda kwa kumkingia kifua Waziri Mkuu na kukiuka Kanuni za Kudumu za Bunge. "Mimi sijashtakiwa mahakamani kwa kosa lolote linalohusu mauaji ya wananchi wa Nyamongo, Tarime na wala kesi yangu katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime haiuhusu matukio ya Nyamongo", Lissu alisema.

Aliongeza kwamba: "Wakati mauaji ya wananchi wa Nyamongo yalifanywa na Jeshi la Polisi tarehe 16 Mei, mimi na wenzangu wengine saba tumeshtakiwa kwa madai ya kuingia kijinai katika eneo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime; kwa kufanya mkusanyo haramu katika eneo hilo; na kwa kuwazuia mganga wa Hospitali hiyo na askari polisi kufanya uchunguzi wa miili ya marehemu Emmanuel Magige, Chacha Ngoka, Chawali Bhoke na Mwikwabe Marwa waliouawa na Jeshi la Polisi. Makosa yote matatu yanadaiwa kutokea mnamo majira ya saa nne usiku wa tarehe 23 Mei 2011."


Kuhusiana na Mbunge Matiko, Lissu alidai kwamba Mbunge huyo wa Viti Maalum hakabiliwi na mashtaka yoyote mahakamani kwa jambo au kosa lolote lile.

"Inaelekea Spika wa Bunge alitoa uamuzi wake huo bila hata kuuliza au kupewa taarifa sahihi kuhusu masuala ya mauaji ya Tarime na kesi iliyofunguliwa dhidi yangu na wenzangu. Hii ni hatari sana kwa uendeshaji bora wa Bunge kama Spika ambaye ndiye kiongozi mkuu wa Bunge atakuwa anatoa maamuzi ambayo hana taarifa sahihi juu yake. Sio tu mijadala inayohusu masuala muhimu kwa umma na ambayo yanatakiwa kujadiliwa Bungeni itazuiliwa kwa hoja zisizozingatia Kanuni za Kudumu za Bunge, bali pia hadhi na heshima ya Bunge na ya Spika mwenyewe itashuka kwa vile wananchi wataona kwamba Spika anafanya maamuzi kwa lengo la kuwakingia kifua mawaziri na Serikali ili wasiwajibishwe Bungeni. Hii ikitokea itakuwa ni hatari sana kwa demokrasia yetu ya kibunge."


Mheshimiwa Lissu alidai kwamba hii si mara ya kwanza kwa Spika Makinda kutoa uamuzi ulioonekana kumkingia kifua Waziri Mkuu wakati wa Kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu. "Itakumbukwa kwamba wakati wa Mkutano wa Pili wa Bunge la Jamhuri uliofanyika mwezi Februari mwaka huu, Mbunge wa Arusha Mjini, Mheshimiwa Godbless Lema aliomba Mwongozo wa Spika kutokana na kauli ya uongo iliyotolewa na Waziri Mkuu kuhusu mauaji ya Arusha. Badala ya kutoa mwongozo alioombwa, Spika wa Bunge alimkemea Mheshimiwa Lema na kumtaka athibitishe kauli yake juu ya uongo wa Waziri Mkuu.

Hata hivyo, Lema alipotoa uthibitisho wake Spika Makinda alizima mjadala huo kwa kukalia uthibitisho wa Mheshimiwa Lema. Hadi leo Watanzania hawajaambiwa chochote juu ya jambo hilo."
Mheshimiwa Lissu alisema kwamba vitendo hivi vya Spika vinakiuka Kanuni za Kudumu za Bunge.

"Kwa mujibu wa Kanuni hizi, Spika wa Bunge ana mamlaka makubwa sana kimaamuzi. Hata hivyo, Spika hawezi akaendesha Bunge kama anavyoona yeye binafsi. Anatakiwa kuzingatia kanuni. Na kanuni kuu anayotakiwa kuizingatia muda wote ni kanuni ya 8 inayomtaka kuendesha shughuli za Bunge na "kutoa maamuzi kwa haki, uadilifu na bila chuki wala upendeleo wowote, kwa kuongozwa na Katiba, Sheria za nchi, Kanuni hizi, Kanuni nyingine zilizopo, maamuzi ya maspika wa Bunge waliotangulia na pia kwa kuzingatia uzoefu pamoja na mila na desturi za mabunge mengine yanayofuata utaratibu wa kibunge unaofanana na unaofuatwa na Bunge la Tanzania."

Kuhusiana na hatua wanazotazamia kuchukua dhidi ya uamuzi wa Spika Makinda wa kukataza maswali yao, Mheshimiwa Lissu alisema kwamba watapeleka malalamiko yao kwa Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge ili uamuzi wa Spika uchunguzwe na Kamati hiyo na kutolewa uamuzi.

"Kwa bahati nzuri, uamuzi Spika kuhusiana na jambo lolote sio wa mwisho kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge letu. Pamoja na kwamba tusingependa kufanya hivyo, lakini kuuachia uamuzi potofu wa Spika wa Bunge usimame itakuwa ni kuweka precedent ya hatari kwa Bunge letu kwani uamuzi huo ukiachwa bila kupingwa unaweza kutumiwa kwa mijadala mingine kwa siku zijazo. Ili kuepuka hili, inabidi tumpeleke Mheshimiwa Spika kwenye Kamati ya Kanuni za Kudumu za Bunge ili uamuzi wake ukajadiliwe na kutolewa maamuzi ya haki. Kazi ya kuandaa malalamiko hayo itakamilika baada ya muda mfupi kwani vielelezo vyote muhimu tayari vimekwishapatikana."


--------------------------------------------------------------
Tundu A.M. Lissu (MB.)
MNADHIMU MKUU, KAMBI RASMI YA UPINZANI

No comments:

Post a Comment