Kutokana na Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Fedha, Mhe. Mustafa Mkullo (Mb), aliyoitoa jana bungeni Dodoma tarehe 08/06/2011, kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012. Kambi ya Upinzani tumeshtushwa na upotoshaji mkubwa wa kitakwimu na kimaudhui uliofanywa na serikali kwa lengo la kuwajengea matumaini hewa wananchi kuwa watapata nafuu ya maisha kupitia bajeti hiyo wakati hali halisi haipo hivyo.
Yafuatayo ni baadhi tu ya maeneo ya waziwazi ambayo serikali ya CCM kupitia kwa Waziri wake Mhe. Mkulo iliamua kuupotosha umma wa Watanzania kwa makusudi kama ifuatavyo;
1. Wakati Waziri akitaja kuwa kipaumbele cha kwanza cha bajeti hiyo ni kumaliza tatizo la Umeme na hivyo kutamka kwamba ametenga shilingi 537 Bilioni, , upembuzi uliofanywa na Kambi yetu ya Upinzani kwenye vitabu vya bajeti (Kitabu Namba II na IV) vilivyotolewa na serikali yenyewe, umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa jumla ya kiasi cha shilingi 402,402,071,000 kwa mujibu wa fungu la 58. Fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya Matumizi kawaida shilingi 76,953,934,000 na kwa upande wa bajeti ya Maendeleo zimetengwa shilingi 325,448,137,000. Shilingi Bilioni 325 zilizotengwa katika Bajeti ya Maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa 160MW, 100 Dar es Salaam na 60 Mwanza. Hakuna mradi wowote mpya wa umeme unaonekana katika Bajeti. Ni dhahiri kuwa kauli ya Mkulo ililenga zaidi kuwajengea wananchi matumaini hewa kuliko kuchukua hatua za kweli za kumaliza tatizo la umeme.
2. Wakati Waziri na Serikali wanataka kuwaaminisha Watanzania kuwa bajeti ya mwaka huu imeongezeka kuliko ilivyokuwa mwaka 2010/2011, ukweli ni kuwa hakuna ongezeko halisia (real term increase) lililofanyika. Bajeti iliyopita ilikuwa kiasi cha shilingi 11.6 trilioni wakati mwaka huu wa 2011/2012 serikali ina bajeti ya jumla ya shilingi 13.525 trilioni. Kati ya ya fedha hizo za mwaka 2011/2012, kiasi cha shilingi 1.901 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 14.06% ya bajeti yote, kitatumika kulipia deni la Taifa. Kwa mantiki hiyo, mtaona kuwa fedha kwa ajili ya kuendesha serikali pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zitabaki kuwa ni kiasi cha shilingi trilioni 11.624 ambazo ni sawa na fedha za bajeti ya mwaka uliomalizika wa 2010/2011 (Japo thamani ya shilingi imeanguka ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka 2010/2011). Tunasisitiza kuwa hii si bajeti ya maendeleo, hii ni bajeti ya madeni.
3. Wakati Waziri akisema Bungeni kuwa Bajeti ya mwaka 2011/2012 itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kuthibiti matumizi, nanukuu “kupunguza malipo ya posho mbalimbali yasiyokuwa na tija (uk.53)”, ukweli ni kuwa Bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012 imetenga jumla ya shilingi 0.987 trilioni ambazo ni sawa na asilimia 13 % ya bajeti yote ya serikali kwa ajili ya kulipa posho chini ya vifungu vinavyojulikana kama “Personnel allowances (non discretionary na In-kind”). Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkulo kuwa serikali itapunguza posho sio kweli. Tunautaka umma wa Watanzania usikubali kurubuniwa.
4. Wakati Waziri akisema kuwa ili kuthibiti matumizi watapunguza posho mbalimbali, kwenye hotuba yake uk.66, waziri amependekeza kufanywa kwa marekebisho ya sheria ya kodi ya mapato SURA 332 na anasema kwenye (i) “kusamehe kodi ya mapato kwenye posho wanazolipwa wafanyakazi wa serikali na wanaofanya kazi kwenye taasisi zinazopata ruzuku kutoka kwenye bajeti ya serikali” . Hii inaonyesha dhahiri kuwa kauli ya Kufuta au kupunguza posho ilitolewa na Serikali ili kupumbaza wananchi lakini haina udhati.
5. Bajeti ya serikali ya mwaka 2011/2012 imewaongezea mzigo mkubwa sana wananchi na haswa wajasiriamali wadogo na vijana ambao wamejiajiri ama kuajiriwa kwenye biashara ya usafiri na usafirishaji. Tunasema hivyo, kwa sababu serikali katika bajeti vyake rasmi vya bajeti imeamua kufanya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani sura 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati mtu akiwa anaendesha gari yaani (Traffic Notification Fee), kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 300,000. Lakini Waziri Mkulo katika Hotuba yake aliyoitoa jana ukurasa 74, alitamka kuwa wataongeza kiwango cha faini hadi kufikia shilingi 50,000. Ni dhahiri kuwa kauli ya waziri ya kusema faini itafikia 50,000 wakati kwenye vitabu rasmi vya bajeti faini hiyo inaonekana itafikia 300,000, hivyo alilenga kuuhadaa umma na kuupotosha.
6. Kambi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na kushangazwa na hatua ya Serikali kutenga zaidi ya robo ya Bajeti kulipa Madeni na Kulipana Posho (Asilimia 27 – 14% kulipa madeni na 13% kulipa Posho mbalimbali).
7. Kambi ya Upinzani itawasilisha Bungeni Bajeti Mbadala siku ya Jumatano tarehe 15.6.2011, saa tano asubuhi ambayo itakuwa inajali masilahi ya Watanzania yenye lengo la kukuza Uchumi wa Vijijini (rural growth) na itajikita katika kupata vyanzo vipya vya mapato na kubana matumizi ikiwemo kufuta Posho mbalimbali.
Imetolewa leo, Mjini Dodoma, na
Zitto Zuberi Kabwe
Waziri Kivuli wa Fedha
Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni
Kutoka Ofisi za Upinzani Bungeni
Regia E Mtema
Waziri Kivuli-Kazi na Ajira
No comments:
Post a Comment