CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemtaka Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, kutoa ufafanuzi wa zaidi ya sh bilioni 220 zilizopotea katika idara mbalimbali ndani ya jeshi hilo.
Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa, mwishoni mwa wiki alipohutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kiwanja cha Kampala, Gongo la Mboto, Dar es Salaam.
"Ninamshauri Mwema kama anataka siasa avue magwanda yake na aje tufanye siasa kwa kuwa sasa ameamua kuisemea serikali, nilifikiri angetumia muda wake kwa ajili ya kutolea ufafanuzi ripoti ya CAG ya April 2010 iliyowasilishwa bungeni Machi na Aprili mwaka huu inayoonyesha kiasi cha zaidi ya bilioni 220 kutojulikana zimetumikaje ndani ya jeshi lake," alisema.
Alisema kati ya fedha hizo, sh milioni 800 zimepotelea katika Jeshi la Magereza peke yake, huku wafungwa walio katika magereza nchini wakikosa huduma zinazostahili ikiwamo kupata chakula bora, na kiasi kilichosalia ni katika idara mbalimbali ya jeshi la polisi.
Aliongeza IGP amekuwa na ujasiri wa kukemea wanasiasa huku akishindwa kuonyesha ujasiri wa kujiuzulu katika nafasi yake kutokana na kushindwa kuchukua hatua kwa maovu yanayofanywa katika maeneo mbalimbali yanayolindwa na jeshi lake, linalopokea kodi ya Watanzania waliofanywa kuwa na hali duni na serikali ya CCM.
"Hivi wizi wote wa EPA, Meremeta na matukio mengine yaliyofanyika maeneo hayo yote si yanalindwa na Jeshi la Polisi? Kwa nini asiyatolee ufafanuzi na badala yake anaona wanasiasa wanataka kuvuruga amani. Kama kuyasema haya ni kuvuruga amani basi ninajua hapa mpo usalama wa taifa na polisi nendeni mkamwambie sisi tutayazungumza kila siku na aje atukamate," alisema Dk. Slaa.
Mbali na hilo, Dk Slaa aliwatahadharisha viongozi wa dini kuepukana na ghilba za jeshi hilo kuwatumia kama kivuli cha kuficha maovu ya serikali iliyo madarakani.
Alisema IGP anaona kitendo cha wanasiasa kuzungumzia upungufu wa serikali iliyo madarakani kama uchochezi, bila kujua vyama hivyo vipo kisheria kwa ajili ya kuikosoa serikali pale inapoenda kinyume na matarajio ya Watanzania.
Akizungumzia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, Dk. Slaa alisema dhana nzima ya Uhuru uliokuwa ukielekezwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa sasa umekuwa ni kama hadithi ya kusadikika.
Huku akinukuu baadhi ya vifungu toka katika kitabu cha 'Binadamu na Maendeleo' kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere, Dk. Slaa alisema Mwalimu alielezea uhuru katika njia tatu ambazo ni Uhuru wa Kujitawala, Uhuru wa kutosumbuliwa na njaa maradhi na umaskini pasipo sababu za msingi na uhuru wa mtu binafsi.
Alisema uhuru wa kutosumbuliwa haupo katika nchi yetu kwa kuwa hii leo kuna maeneo mengi watu wanataabika kwa njaa, maradhi na umaskini uliokithiri huku serikali ikijinadi kwa takwimu zisizoweza kumsaidia Mtanzania wa hali ya chini.
"Mwalimu alisema katika kitabu chake hiki (anakionyesha kitabu hicho) na hii ilikuwa ni hotuba yake ya mwaka 1968 kuwa maendeleo si kuwa na takwimu za ujenzi wa barabara, nyumba nyingi na mazao hizo ni nyenzo za kuendea maendeleo, sasa tuangalie haya yanayosemwa ni maendeleo kama yamemnufaisha Mtanzania aliyeko vijijini?" alihoji Dk. Slaa.
Aidha, alisema maadili ya uongozi nchini yaliondoka enzi ya utawala wa Nyerere na Rais Ali Hassan Mwinyi, hivyo kusema tunaadhimisha miaka 50 ya uhuru bila kuwa na mlingano wa mapato na kile kinachoitwa maendeleo ni kujidanganya.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Zanzibar, Said Issa Mohamed, aliwataka Watanzania wasihadaike na kelele zinazopigwa kwamba kuna vyama vya upinzani vina ajenda ya udini, kwa kile alichokieleza kuwa ni propaganda zinazotumiwa kwa lengo la kuwagawa Watanzania wasizungumzie matatizo yao.
Alisema hali ngumu inayopigiwa kelele na vyama vya upinzani ni kwa manufaa ya watu wote bila kujali dini zao na kwamba inahitajika nguvu ya pamoja kwa ajili ya kutetea maslahi ya taifa. Source: Tanzania Daima

No comments:
Post a Comment